Friday, December 2, 2011

KOCHA WA SIMBA AWAUZA OKWI NA KAZIMOTO ULAYA....

Milovan Cirkovic ‘Profesa Chico’.

KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic ‘Profesa Chico’, amesema wachezaji wake wawili, kiungo Mwinyi Kazimoto na Emmanuel Okwi, wana nafasi ya kucheza soka barani Ulaya.
Prof Chico alimshuhudia Kazimoto katika mechi dhidi ya Djibouti lakini akalazimika kumsaka Okwi kwenye mtandao baada ya kusikia amefunga mabao matatu katika mechi moja ‘hat-trick’.
                                                   Mwinyi Kazimoto

                                                  Emmanuel Okwi

“Baada ya kumuona Okwi, nimefurahi sana kugundua ana kiwango kizuri kama nilivyokuwa nikielezwa. Najua kila kitu nitapanga nitakapokutana nao na kuanza kazi lakini ni wachezaji wanaoweza kucheza Ulaya.

“Ninaamini Simba ina wachezaji wengi wa aina hiyo, bado naendelea kuwaangalia wengine na nitaenda kuangalia mechi karibu zote za Kombe la Chalenji kwa ajili ya kuona wachezaji wangu, wa timu pinzani na wengine,” alisema Prof Chico, raia wa Serbia, aliyechukua nafasi ya Mganda, Moses Basena.

Kazimoto alionyesha kiwango cha juu katika mechi kati ya Kilimanjaro Stars dhidi ya Djibouti ikiwa ni pamoja na kufunga bao safi katika ushindi wa mabao 3-0.

Mserbia huyo amesisitiza, anataka kuona kikosi chake kinacheza mpira wa kuvutia kabla ya kuanza kusaka mabao.
“Mkicheza pasi za uhakika ni rahisi kutimiza malengo. Angalia wanavyofanya Barcelona au hata Arsenal, nataka tucheze vile,” alisema Mserbia huyo.

No comments:

Post a Comment