Serikali itake Israel waombe radhi; tukijiheshimu, tutaheshimiwa
Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya
Kimataifa ya CHADEMA inaitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa
tamko juu ya kauli ya Waziri wa Ulinzi wa Israel ya kwamba nchi yetu si ya
muhimu wala ya maana.
Waziri Barak alifanya mahojiano na Radio Israel
na kutoa kauli ambayo imenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari vya nchi hiyo
wiki iliyopita kuwa “ Germany, France and England are not Tanzania, Mauritania
or Tripolitania…..these are very important, very relevant countries and we don’t
have an interest in increasing tensions with them or making them bitter
enemies”.
Kwa kauli hii serikali ya Israel inaiona
Tanzania sio nchi ya muhimu wala ya maana hata kufikia hatua ya kuilinganisha na
eneo tu ndani ya Libya linaloitwa Tripolitania.
Tunamtaka Waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano
ya Kimataifa, Benard Membe kuitaka serikali ya Israel kuomba radhi kufuatia
kauli hiyo au kueleza wazi iwapo mazungumzo hayo ya Waziri Barak ni msimamo wa
nchi hiyo kuhusu uhusiano wa kidiplomasia wa mataifa yetu.
Barua pekee ya balozi wa heshima wa Tanzania
nchini Israel, Kasbian Nuriel Chirich kwenda kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa
Israel Avigdor Lieberman ya kulaani matamshi hayo ya Waziri Barak na
kumkaribisha mwakilishi wa Israel kutembelea Tanzania haitoshi kuifanya serikali
ya nchi hiyo kutambua athari za kidiplomasia za kauli iliyotolewa.
Aidha kwa kuwa serikali imekuwa ikieleza kwamba
Tanzania ina mahusiano mazuri ya kiulinzi na Israel, ni muhimu pia Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dr Hussein Mwinyi akaeleza umma iwapo kauli
hiyo ya Waziri Barak ndio msingi wa mahusiano yaliyopo kati ya nchi zetu kuhusu
ulinzi na usalama.
Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya
Kimataifa inachukua fursa hii kurudia kuwakumbusha watanzania kwamba kupuuzwa
huku kwa nchi yetu katika medani ya kimataifa kunatokana na sera mbovu ya mambo
ya nje chini ya utawala wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tanzania imepoteza heshima katika siasa za
dunia kutokana na diplomasia yetu kujikita katika kuomba omba kimataifa; pamoja
na kuwa kimaneno na maandishi serikali inazungumza kuhusu diplomasia ya
kiuchumi, kivitendo mahusiano yetu yamejengeka katika misingi ya utegemezi,
kupungua kwa urari wa kibiashara na kuachia mianya ya uporwaji wa
rasilimali.
Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya
Kimataifa inatambua kwamba wakati wa uongozi wa awamu ya kwanza wa hayati
Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania ilikuwa na heshima na sauti kimataifa sio tu
katika jitihada za ukombozi kusini mwa Afrika bali pia katika mahusiano ya
kisiasa, kiuchumi na kijamii baina ya nchi za kusini na mataifa mengine
duniani.
Hali ya Tanzania kupoteza sauti katika medani
ya kimataifa imedhihirika pia hivi karibuni katika mkutano kuhusu mabadiliko ya
tabia nchi (COP 17) uliomalizika hivi karibuni nchini Afrika Kusini; wakati nchi
yetu ikiwa ni miongoni mwa waathirika wakubwa zaidi wa mabadiliko ya tabia nchi.
Iwapo hatua hazitachukuliwa kurejesha heshima na sauti ya Tanzania kimataifa
maamuzi mengi yatafanyika yenye athari kwa wananchi wengi bila ushiriki wao
thabiti kama yanayoendelea hivi sasa kuhusu Mikataba ya Kiuchumi na Nchi za
Jumuia ya Ulaya (EPA) yenye madhara kwa wakulima na wenye viwanda nchini.
Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya
Kimataifa inatoa mwito kwa watanzania kuendelea kuunganisha nguvu ya umma
kusimamia uwajibikaji na kufanya mabadiliko ya kimsingi ya kiuongozi, kisera na
kimfumo ya kitaifa ili kuweza kurejesha nafasi na heshima ya Tanzania kimataifa
katika mazingira ya sasa ya ushindani wa kiuchumi, kiulinzi, kijamii na
kisiasa.
Kauli ya Waziri Barak nimuendelezo tu wa
mataifa mbalimbali kuifanya Tanzania na baadhi ya nchi nyingine za Afrika kuwa
hazina heshima wala sauti katika siasa za kimataifa kama ambavyo Serikali za
Uingereza na Marekani zimeweka masharti yenye mwelekeo wa ukoloni mamboleo
kuhusu masuala ya ushoga na usagaji.
Hatua za kupinga kauli za kudharauliwa na
kulazimishwa mambo tusiyoyataka ziende sambamba na kudhibiti mianya yote ya
ufisadi wa kimataifa, uwekezaji uchwara na kutetereka kwa misingi wa utawala wa
kisheria masuala ambayo yanasababisha migogoro na pia rasilimali za nchi
kutokutumika kwa manufaa ya wananchi walio wengi; tukijiheshimu,
tutaheshimiwa.
Wenu katika Demokrasia na Maendeleo,
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya
Kimataifa (CHADEMA)