Friday, July 1, 2011

UJERUMANI YAKUBALI KUTOA MISAADA KWA WAPINZANI WA GADDAFI…!!!

Wanawake wakiwa katika mji wa Tripoli Libya ambayo sasa hivi iko katika mgogoro mkubwa wa kisiasa.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amekutana na kiongozi wa kundi la waasi nchini Libya, mjini Berlin, kujadili usaidizi zaidi kwa waasi hao.
Serikali ya Ujerumani imeamua kutoa usaidizi wa kisiasa, kidiplomasia, na fedha katika jitihada za kuendeleza upinzani dhidi ya kiongozi wa Libya, Kanali Muammer Gaddafi.
Westerwelle amesema hili linajumuisha mali zinazomilikiwa na utawala wa Gaddafi zilizopo katika benki za Ujerumani, zinazokisiwa kufika zaidi ya euro bilioni 7.
Kiongozi wa kundi hilo la waasi, Mahmud Jibril, amesema kuwa anaheshimu uamuzi wa Ujerumani kutoshiriki katika operesheni ya shirika la kujihami NATO, kuwalinda Walibya, lakini anashukuru uungaji mkono wa nchi hiyo kwa kulitambua baraza la kitaifa la mpito, na kwa kutoa usaidizi wa aina nyingine.
Serikali ya Ujerumani hapo awali ilikubali kutoa silaha kwa mashambulio ya angani ya NATO nchini Libya.

No comments:

Post a Comment