Thursday, August 25, 2011

AU kuchangisha pesa za janga la njaa


Viongozi wa Afrika wanakutana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kuchangisha pesa ili kukabiliana na mzozo wa kibinadamu unaokabili eneo la pembe ya Afrika.

Mkutano wa leo ulitarajiwa kufanyika wiki mbili zilizopita, lakini ukaahirishwa ili kuupa Muungano wa Afrika muda zaidi kuandaa mkutano huo.
Dola millioni moja na nusu zaidi zinahitajika kukabiliana na janga la njaa, linaloathiri nchi tano barani Afrika. Somalia ambako mzozo wa kisiasa bado unaendelea ndiyo iliyoathirika zaidi .
Mkutano huu wa kuchangisha fedha ni wa kwanza wa aina yake kufanywa na Muungano wa Afrika.
Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, Jean Ping, amesema juhudi za muungano huo hazitoshi na madhumuni ya mkutano huu wa siku moja ni kuchangisha dola billioni moja na nusu kufadhili janga hilo.
Nchi kadhaa za Afrika tayari zimetoa michango yao katika juhudi hizo za kibinadamu, lakini muungano huo umeshutumiwa kwa kuchelewa kushughulikia janga hilo kwa haraka.
Hata hivyo, Muungano huo umejitetea na kusema ulihitaji muda zaidi kushirikiana na wanachama wake na kuandaa mkutano.
Waandalizi wa mkutano huu wanasema mkutano wenyewe hautachangisha pesa pekee , lakini pia viongozi watajadili suluhu za kudumu za kukabiliana na majanga ya kibinadamu barani Afrika.

No comments:

Post a Comment