Friday, June 3, 2011

Al-Qaeda wamtangaza mrithi wa Osama



Islamabad, Pakistani
KUNDI la Al-Qaeda limemteua mwanajeshi msataafu wa Misri, Saif Al-Adel kuwa kiongozi wake wa mpito baada aliyekuwa akiliongoza, Osama bin Laden kuuawa na makachero wa Marekani Mei 2, mwaka huu.

Osama aliuawa na makachero hao wa kikosi maalumu baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Abbottabad, Kaskazini mwa Pakistani na mwili mwake kuzikwa baharini muda mfupi baada ya mauaji hayo.

Kama alivyokuwa Osama, Al-Adel ni miongoni mwa viongozi wa Al-Qaeda walio kwenye orodha ya wanaosakwa na Serikali ya Marekani ama wakiwa hai au wamekufa.

Taarifa ya Al-Qaeda iliyosambazwa jana kwenye vyombo vya habari, imeeleza kuwa Al-Adel ataliongoza kundi hilo kwa muda, akisaidiwa na aliyekuwa msaidizi wa bin Laden, Ayman al-Zawahri.

‘’Yeye siyo kama ni kiongozi kamili, bali ataongoza katika kipindi hicho cha mpito hasa katika oparesheni za kijeshi," ilisema taarifa hiyo iliyonukuliwa na Shirika la Habari la

Al–Adel anatuhumiwa na Marekani kuwa ndiye aliyehusika kuzilipua kwa mabomu balozi zake za mjini Nairobi- Kenya na Dar es Salaam mwaka 1998.

Kiongozi huyo mpya wa Al-Qaeda, aliwahi kuwa mkuu wa kamati ya kijeshi ya kundi hilo baada ya kifo cha Mohammed Atef mwaka 2001.

"Katika miaka ya 1990, Al- Adel alikuwa anafanya kazi Iran," imesema taarifa hiyo.
Imeelezwa pia kuwa Al-Adel ndiye aliyekuwa mratibu wa mashambulizi yaliyofanywa na kundi la Al-Qaeda nchini Morocco Mei, 2003.

Jeshi la Pakistani lalalamika
Jeshi la Pakistani limewasilisha  malalamiko kwa Jumuia ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (Nato), baada ya wanajeshi wake wawili kujeruhiwa katika makombora yaliyorushwa na majeshi ya jumuia hiyo juzi katika mpaka wa Afghanistani.

Katika taarifa yake jana, jeshi hilo limesema helikopta hizo za Nato zilikiuka uhuru wa anga ya Pakistani. Nato haijatoa taarifa juu ya tukio hilo.

Hata hivyo, ofisa mmoja wa jumuia hiyo, aliliambia Reuters kwa sharti la kutotajwa jina kwamba helikopta hizo ziliishambulia Pakistani baada ya kushambuliwa katika mpaka wa Afghanistani.

Maofisa wa Pakistani wamedai kuwa tukio hilo linaweza kuongeza msuguano ulioanza kujitokeza kati ya Marekani na nchi hiyo baada ya mauaji ya bin Laden.

No comments:

Post a Comment