Friday, June 3, 2011

Kashfa za rushwa zaendelea kuisumbua FIFA


ZURICH, Uswisi
MAKAMPUNI makubwa mawili yanayolidhamini Shirikisho la Soka Duniani FIFA yameonyeshwa kusikitishwa na tuhuma za rushwa zinazotolewa kwa taasisi hiyo huku rais wa FIFA, Sepp Blatter akikataa kukubali kuwa Shirikisho hilo kuwa katika matatizo katika kipindi hiki.

Taarifa ya kampuni wa Coca Cola ilisema,"tuhuma hizi za rushwa kwa FIFA zinahuzunisha na pia ni mbaya kwa mchezo wa soka."Wakati Coca Cola wakitoa taarifa hiyo, kampuni la Adidas lenyewe lilisema,"migogoro na suala la rushwa yote hayo yanaumiza mchezo wa soka."

Akizungumza katika makao makuu ya FIFA mjini Zurich, raisi wa FIFA, Sepp Blatter alisema,"Soka haipo katika migogoro hivi sasa, ila soka inapitia katika kipindi kigumu hivi sasa na sisi familia ya soka ndiyo tutakao maliza kipindi hicho kigumu."

Kipindi cha hivi karibuni zimeibuka tuhuma za rushwa katika kampeni za kuwania uongozi wa FIFA, pia zimeibuka tuhuma za rushwa katika utoaji wa zabuni za kuandaa Fainali za Kombe la Dunia.

Katika siku chache zilizopita, nchi ya Qatar imeshutumiwa kwa kutoa rushwa na hivyo kufanikiwa kushinda zabuni ya kuandaa Fainali za Kombe la Dunia 2022, wakati raisi wa Shirikisho la Soka barani Asia,  Mohamed Bin Hammam na raisi wa CONCACAF, Jack Warner wameondolewa kataika nafasi za uongozi wa FIFA kwa tuhuma za rushwa.

Kutokana na hali hiyo Bin Hammam ambaye alikuwa mpinazani wa Blatter katika kuwania nafasi ya uraisi wa FIFA alijitoa katika nafasi hiyo siku ya Jumatano na hivyo kubaki Blatter peke yake akiwania nafasi hiyo.

Makampuni ya Coca-Cola na Adidas yote yameonyesha kutofurahishwa na taarifa za rushwa ndani ya FIFA kwa sababu makampuni yote mawili ni marafiki wa FIFA, ambapo makampuni hayo hutoa fedha, vitu mbalimbali na huduma mbalimbali na zaidi hufanya katika Fainali za Kombe la Dunia ili yaweze kufahamika sehemu mbalimbali duniani kupitia matangazo.

"Tunatarajia FIFA watalishughulikia suala hili kwa hekima na busara na kuhakikisha wanalimaliza suala hili la rushwa lililojitokeza katika Shirikisho hilo,"alisema msemaji wa kampuni ya Coca Cola, Petro Kacur.

Naye msemaji wa kampuni ya Adidas alisema,"hili suala la rushwa katika FIFA ambalo hivi sasa linazungumzwa katika jamii siyo zuri kwa mchezo wa soka na pia siyo zuri kwa FIFA na washirika wake."Hata hivyo Adidas imesema itaendeleza ushirikiano wake na FIFA ambao imeanza nao miaka 30 iliyopita.

Wakati huo huo makamu wa raisi wa Shirikisho la Soka la barani Asia,Zhang Jilong amesema Mohamed bin Hammam bado ni raisi wa Shirikisho la Soka barani Asia, huku akisema FIFA haina mamlaka ya kumtoa madarakani kiongozi huyo wakati kiongozi huyo hivi sasa anafanyiwa uchunguzi wa tuhuma kwamba alinunua kura ili achaguliwe kuongoza Shirikisho hilo la Soka Duniani.

Jumapili iliyopita FIFA ilimuondoa Mohamed bin Hammam kwenye shughuli zote za michezo.

No comments:

Post a Comment